Huu pichani kushoto ni ukumbi wa mikutano wa manispaa ya mji wa Tabora ambao umepewa jina la Mtemi Isike Mwana Kiyungi, ukumbi huo ambao utafunguliwa rasmi baadae mwaka huu, umepewa jina hilo kama ishara ya kumuenzi Mtemi huyo wa 12 wa himaya ya Unyanyembe ambaye alipigana na Wajerumani kwa takriban miaka mitano ambapo walipoivamia ngome yake iliyoitwa Ishinula huko Itetemia maili tano toka Tabora mjini alijilipua kwa baruti kuliko kukamatwa na Wajerumani. Miaka ya nyuma kumbukumbu pekee ya Mtemi Isike ilikuwa ni shule ya msingi na tawi la benki ya NBC Tabora mjini. Kinyume na Mtemi Isike, Mirambo ambaye hakuwa mtemi wa kijadi kama Isike bali mnyanganyi wa pembe za ndovu na bidhaa nyingine zilizopitishwa maeneo ya Urambo na Waarabu amepewa heshima kubwa na serikali ya Tanzania kiasi cha kuibatiza minara pacha ya Benki kuu ya Tanzania jina la Mirambo. Huu ni mfano tu wa jinsi serikali za awamu zote ambavyo huko nyuma hazikuthamini michango mbali mbali ya viongozi wetu wa kabla na baada ya uhuru.
0 comments :
Post a Comment