Mh John Mnyika Mbunge wa Ubungo akisisitiza kitu |
Mh Paul Makonda, mkuu wa wilaya mpya Kinondoni. |
UAMUZI wa Rais Jakaya Kikwete kumteua Katibu wa Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Paul Makonda umeibua gumzo na mijadala kila kona ya nchi huku Mbunge wa Ubungo John Mnyika (Chadema), akimtumia ujumbe maalumu.
Makonda ambaye pia alikuwa mbunge wa Bunge Maalumu la Katiba ameteuliwa na rais kushika wadhifa huo juzi ambapo pia wapo wakuu wa wilaya wengine 26 wapya.
Pia, Rais Kikwete katika mabadiliko ya wakuu wa wilaya hayo, wapo ambao amewabadilisha vituo vya kazi na wengine wakiachwa. Hata hivyo pamoja na kuteuliwa kwa wakuu wa wilaya wapya 27, gumzo kubwa limebaki kwa Makonda ambaye anaonekana kama mwanasiasa kijana machachari kwenye medani ya siasa nchini.
Mnyika alisema jana kuwa kitendo cha rais kumteua kijana huyo ni ujumbe tosha kwa Jaji mstaafu, Joseph Warioba na wengine kuwa Serikali inafurahishwa na vitendo vya ukosefu wa maadili.
“Watanzania wanakumbuka tukio la kufanyiwa vurugu kwa Jaji Warioba eneo la Ubungo Plaza Dar es Salaam na miongoni mwa wanaotuhumiwa kumfanyia vurugu mzee Warioba ni Makonda.
“Leo hii tunashangaa anateuliwa kuwa DC wa Kinondoni. Hii maana yake ni moja tu hata ukiwa na utovu wa nidhamu, Serikali ya CCM itakufurahia na kukupa nafasi na ndicho ambacho kimetokea kwa Makonda,”alisema Mnyika.
Alisema iwapo vurugu zilifanywa kwa Jaji Warioba maana yake ni moja tu hata wapinzani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu watafanyiwa vurugu na akina Makonda na wenzake wengine waliopewa nafasi hizo.
“Inaonesha wazi, Makonda ameteuliwa kwa ajili ya kufanya vurugu maana alianza kufanya hivyo kwa Jaji Warioba na badala ya Serikali ya CCM kukasirishwa imeamua kumpa nafasi ili aendelee na utovu wake wa nidhamu,”alisema.
Kwa maoni yangu napenda kuamini kuwa Rais Kikwete lazima anajua kupitia vyombo vya usalama kuwa Paul Makonda hakuhusika na kumfanyia fujo Mh Warioba ndio maana akampa ukuu wa wilaya kijana huyo.
Habari na picha kwa hisani ya Magendela Hamisi na Nyendo Mohamed wa Jamboleo
0 comments :
Post a Comment